DHUMUNI LA MUNGU KUMUUMBA MWANADAMU (MTU)

Dhumuni ni nini?
Dhumuni ni lengo,kusudi, au waweza kusema msukumo unapelekea (sababisha)kufanyika kwa jambo Fulani(mf: katika uandishi wa barua.)

Mungu ni nani?
Mungu ni muumbaji wa sayari zote ikiwemo na dunia na vitu vyote vinavyo onekana kwa macho ya kawaida (nyama) na vile vyote visivyo_onekana kwa macho ya kawaida.(soma biblia katika kitabu cha mwanzo:SURA 1-2 zote.) Mungu ni mweza wa yote (mwenyezi Mungu) Yeremia 32:27 Inasema , "Tazama mimi ni Bwana,Mungu wa wote wenye mwili, je, kuna neon lolote nisiloliweza?" Mungu ni Roho iliyo hai iliyokuwepo tokea kale (mwanzo)na sasa bado ipo na tena itaendelea kuwepo daima na milele. Ufunuo wa yohana 1:8 Inasema,Mimi ni Alfa na Omega,mwanzo na mwisho ,asema Bwana Mungu aliyeko na aliyekuwako na atakayekuja, mwenyezi."

Kuumba ni nini?
Kuumba ni kutengeneza au waweza kusema ni uundaji wa kitu unaotokana na ubunifu wa muundaji. Hii ina maana kwamba kabla ya muundaji hajabuni kuunda hicho kitu hakikuwepo kabisa.

Kwa kunzingatia ufafanuzi wa maelezo yaliyotangulia hapo juu , hii inamaanisha ya kwamba kabla Mungu hajabuni kumuunba mwanadamu huyu mwanadamu hakuwepo kabisa. Hivyo basi hihi ni wazi kuwa kutokana na wazo,ubunifu na hatimaye uumbaji wa Mungu ndiko kuliko peleke kuwepo kwa kiumbe anayeitwa mwanadamu katika dunia ya leo.

Mwanadamu ni nini?
Mwanadamu ni jina lililotokana na kiumbe wa kwanza aliyeumbwa kwa sura na mfano wa Mungu na Mungu ndiye aliyemwita kiumbe yule wa kwanza jina lake kuwa ni Adamu.( Mwanzo 5:1-2) biblia inasema, Hiki ndicho kitabu cha vizazi vya Adamu. Siku ile Mungu aliwaumba, akaawabariki akaawaita jina lao Adamu; siku ile walipoumbwa."

Baada ya uumbaji huu wa Adamu; Adamu aliendelea kuzaa watoto, na hao watoto wakaitwa watoto wa Adamu na ndio maana leo hii sisi tunaitwa Wana wa Adamu (Wanadamu).

Na hili neon Asamu asili yake ni katika lugha ya kiebrania (kutoka taifa la Israeli) na maana yake ni Usongo mwekundu. Kwa hiyo sisi tunaoitwa wanadamu maana yake ni wana wa udongo mwekundu.

Katika maelezo ya kichwa cha habari cha somo hili nimeandika Dhumuni la Mungu kumuumba Mwanadamu na baada ya neno Mwanadamu katika parandesi nikaandika neno jingine yaani mtu. Kwa matazamo wa haraka watu wengi wanajua ya kwamba Mwanadamu na mtu ni kitu kimoja; lakini ukweli wenyewe ni kwamba Mwanadamu si mtu na mtu si mwanadamu.

Kama nilivyokwisha kueleza hapo awali tafsiri kamili na sahihi ya jina Mwanadamu; nataka utambue sasa, kuwa Mwanadamu ni jina analoitwa mtu. Yaani hii in maana mtu ndiye kiumbe hai aliyeumbwa na Mungu na Mwanadamu ndilo jina analoitwa huyo mtu.

Zingatia ya kwamba

Mtu ni kiumbe hai Mwanadamu ni jina la huyo kiumbe hai.
Kwa mfano:- Ukisikia mtu anaitwa jina lake Mussa hii ina maana ya kwambal; yuko kiumbe hai ambaye jina lake ndilo hilo Mussa. Yaani hii inaonyesha wazi kuwa Mussa ni jina tu na wala sio kiumbe hai.

Mtu ni nani?
Mtu ni kiumbe hai aliyeumbwa na Mungu kwa sura na mfano wa Mungu. Mwanzo 1: 26 a , b na c Inasema; Mungu akasema, Na tufanye mtu kwa mafano wetu, kwa mfano wetu, kwa sura yetu.

Na huyu mtu aliyeumbwa kwa mfano wa Mungu na sura yake ikiwa kama Mungu alivyo amegawanyika katika sehemu kuu tatu ambazo ni :
  1. Roho
  2. Mwili
  3. Nafsi
Sehemu zote tatu za huyu mtu Mungu ameziumba kwa makusudi maalum.

Roho ni nini?
Roho ni pumzi ya Mungu ndani ya Mwanadamu au waweza kusema Roho ni uhai wa Mungu ulio ndani ya Mwanadamu. Na makusudi ya Mungu ya kuumba hii Roho ni ili iweze kumwabudu yeye tu na wala si kitu kingine.
Yohana 4:24 Inasema Mungu ni Roho, nao wamwabuduo yeye imewapasa kumwabudu katika roho na kweli."

Kwa mujibu wa andiko hili Biblia ina tufundisha kuwa mungu yeye ni roho na sisi tunaotaka kumwabudu imetupasa kumwabudu katika roho kwa sababu tendo la kuabudu lipo katika roho tu na wala si sehemu nyingine ya mwanadamu. Hivyo ni wazi kabisa kazi ya roho ya mwanadamu ni kumwabudu mungu tu wala sio kufanya neno lingine

Mwili ni nini?
Mwili ni nyumba(jengo) inayotumika katika kuifadhi roho ya mtu au waweza kusema ni maskani ya Mungu. Mwanzo 2:7 inasema Bwana mungu akamfanya mtu kwa mavumbi ya ardhi, akampulizia puani pumzi ya uhai mtu akawa nafsi hai"
Hapa Biblia inatufundisha ya kwamba mwili wa mwanadamu umeumbwa kutokana na mavumbi ya ardhi(udongo) baada ya kuumbwa huu mwili ulikuwa hauna uhai, lakini baada ya mungu kupulizia pumzi yake puani mwa huu mwili ndio ukaweza kuwa nafsi hai. Hii inatuonyesha kuwa baada ya pumzi ya mungu kuingia ndani ya huu mwili na kukaa humo mwili ukawa hai kwa kuzingatia hilo ni dhahiri kuwa mwili ni nyumba au maskani ya pumzi ya Mungu. Na hii pumzi ya mungu ndio roho ya mtu kwa kufuata maan halisi ya roho inayosema roho ni pumzi ya mungu ndani ya mwanadamu na ikiwa roho inakaa ndani ya mwili basi huu mwili ni nyumba ya kuhifadhia roho ya mtu .

Na makusudi ya mungu ya kuumba huu mwili ni ili uweze kumtukuza yeye tu wala sio kitu kingine. 1Wakorinto 6:19-20 inasema, Au hamjui ya kuwa mwili wenu ni hekalu la roho mtakatifu aliye ndani yenu mliyepewa na mungu ? wala ninyi si mali yenu wenyewe, maana mlinunuliwa kwa thamani. Sasa basi mtukuzeni mungu kwa miili yenu. Biblia inatufundisha kuwa mungu ametupa mwili ili tumtukuze yeye mungu peke yake kupitia miili yetu. Mungu anataka kuona sisi tukimtukuza yeye kupitia miili yetu kwa njia ya kutenda mema kwa wakati wote tutakapo kuwa hapa duniani.

Mungu hapendi na anachukia sana kuona tuna tumia miili hii kuona tunatumia miili hii aliyotupa kwa kuimba au kucheza nyimbo zisizompa utukufu na kunamambo mengi ambayo mwanadamu hufanya kinyume na makusudi ya mungu kama vile ulevi uzinzi uasherati nk. Haya yote siyo malengo ya mungu kufanyika kupitia mwili alioumba yeye.

Nafsi ni nini?
Nafsi ni sehemu ya mtu ambayo hiyo ni kiungo kinachounganisha roho na mwili wa mtu. Ndani ya hii nafsi ndiyo kuna kitu kinachoitwa; utashi, hiyari au uamuzi matakwa nk

Utashi, hiyari, uamuzi, na matakwa ni nini?
Hii ni hali ya uchaguzi ambayo imo ndani ya mtu mwenyewe aliye umbwa kwa mfano wa mungu.na hapo katika nafsi ndipo palipo na shida kwasababu ndio kiini cha maamuzi yote.

    Kwa Mfano
  • katika maisha yako umtumikie mungu
  • katika maisha yako umtumikie shetani(ibilisi)
Na makusudi ya Mungu kuumba hii nafsi ni hili iweze kumuhimidi yeye tu na si kitu kingine

Kuhimidi ni nini?
Kuhimidi ni kusifu na kushukuru kwa hiyo nafsi ya mtu inakazi moja tu nayo ni kumsifu na kumshukuru Mungu aliyeiumba
Zaburi 103:1-4
Inasema ee nafsi yangu umuhidi Bwana naam vyote vilivyo ndani yangu viliimidi jina lake takatifu. Ee nafsi yangu umhimidi Bwana, Wala usizisaau fadhili zake zote. Akusamehe maovu yako yote Akuponya magonjwa yako yote, Aukomboa uhai wako na kaburi , Akutia taji ya fadhili na rehema
Hapo biblia ina tufundisha ya kwamba nafsi zetu zina wajibu wa kumhimidi Bwana mungu wetu kwa sababu tuna ishi tukiwa hai mpaka sasa kutokana na fadhili zake Mungu. Hii ina tufundisha kuwa wale wote waliokufa sio kwamba wametenda maovu mbele zake mungu bali ni mapenzi ya mungu wao kuondoka duniani na wewe kuwepo hai.hivyo kwa kutambua hilo inakupasa mwanadamu kumsifu na kumshukuru mungu kwa upendeleo aliokupa wewe kuwepo hai mpaka sasa

Tunasema nafsi ni kiungo kwa sababu ndio inayochukua taarifa za rohoni na kuleta mwilini na kuchukuwa isia za kimwili na kupeleka rohoni na kisha ndipo mtu hutoa maamuzi.

Mfano :-
Mtu anapoubiriwa habari za maisha ya umilele wa baadaye waweza kuwa mzuri ukiamua kuokoka ; na waweza kuwa mbaya usipo okoka ; roho yake inatamani kuokoka ili iepuke adhabu ya kwenda Jehanamu na taarifa hii hutoka katika roho ya mtu itapelekwa katika mwili wa mtu kupitia katika nafsi yake ; na mwili wa huyo mtu utatoa isia zake ya kwamba unaona aibu (haya) au nitakula nini nikiokoka kwasababu shughuli zangu si za halali na hisia izi pia nafsi ya mtu huzichukuwa na kupeleka taarifa zake rohoni na matokeo yake anabaki akisitasita kuokoka

    Mungu alimuumba mtu akiwa mkamilifu katika roho, mwili na nafsi kwa malengo makuu matatu ambayo ni

  • Atawale vitu vyote vilivyomo ndani ya dunia Mwanzo 1:26 inasema na tufanye mtu kwa mfano wetu , kwa sura yetu , wakatawale samaki wa baharini, na ndege wa angani,na wanyama, na nchi yote pia,na kila chenye kutambaa kitambaacho juu ya nchi.

  • Ashilikiane nae (yaani waishi wote kwa pamoja wakiwa na furaha na amani) Mwanzo 3:8-10 Inasema, "Kisha wakasikia sauti ya Bwana Mungu, akitembea bustanini wakati wa jua kupunga; Adamu na mkewe wakajificha kati ya miti ya bustani, Bwana Mungu asiwaone. Bwana Mungu akamwita Adamu, akamwambia, "uko wapi?" Akasema, "Nalisikia sauti yako bustanini, nikaogopa kwa kuwa mimi ni uchi; nikajificha;

    Hii inatuonyesha wazi kuwa kumbe Bwana Mungu alikuwa amemuumba mwanadamu kwa kusudi la kuishi nae pamoja na kushikirikiana nae kwa sababu biblia inatuambia wakati wa jua kuunga Mungu alikuwa ana kawaida ya kwenda katika bustani ya edeni na kuzungumza na mwanadamu aliyemuumba kwa sura na mafano wake mwenyewe.l

    Lengo hili la Mungu lilivurugika baada ya mwamadamu kumuasi Mungu (kutenda dhambi), lakini Mungu bado ana makusudi ya kulitimiza lengo lake hili la kuishi pamoja na mwanadamu aliyemuumba ndio maana kwa Imani twjua watu wote watakao ishi maisha matakatifu watapata nafasi ya kuishi mbinguni na Mungu milele baada ya dunia hii na mambo yake yote yasiyo mpendeza Mungu kupita.
"Tazama, maskani ya Mungu ni pamoja na wanadamu! Naye atafanya maskani yake pamoja nao, Nao watakuwa watu wake. Naye Mungu mwenyewe atakuwa pamoja nao

Pamoja na Mungu kumuumba mtu akiwa na makusudi au malengo yake maalum; bado yeye Mungu ni Mungu wa haki wala sio dikteta. Ndio maana akaweka kitu Utashi yaani maamuzi katika nafsi ya mtu. Na hii hali ya kuwa huru kwa mtu kuchagua ya kwamba awe mtii kwa Mungu au awe mkaidi ndio chanzo cha wengine kwenda Jehanamu na wengine kwenda Mbinguni.

lakini nataka nikutie moyo wewe uliyekubali kumtumikia Mungu kwamba usikate tamaa kwa kuwa hakuna kazi isiyokuwa na mshahara. Warumi 6:23 Inasema; "Kwa maana mashahara dhambi ni mauti; bali karama ya Mungu ni uzima wa milele katika kristo Yesu Bwana wetu.

Hili andiko linatuwekea bayana kuwa wewe uliye amua kumtumikia Mungu hapa duniani na kuacha starehe zote pamoja na anasa zote za dunia hii, utalipwa na Mungu uzima wa milele Mbinguni lakini mtu yule aliyeamuakuishi maisha ya kutenda dhambi ni wazi pia kuwa nayeye anasubiri mashahara wake wa kwenda Jehanamu.

Pia kitabu cha 1 Wakorinto 15:58 KINASEMA; "Basi ndugu zangu wapendwa, mwimarike msitikisike, mkazidisana kutenda kazi ya Bwana siku zote, kwa kuwa mwajua ya kwamba taabu yenu siyo bure katika Bwana."

Nimekwisha kukwambia hakuna kazi isiyokuwa na mshahara. Ujue wazi kuwa ukifanya kazi Tanzania Revenue Authority (T.R.A) ujue mshahara wako wewe upo T.R.A na kama ukifanya kazi shirika la Usafiri Dar-es salaam (UDA) ujue wazi mshahara wako wewe upo UDA. Sasa cha ajabu watu kuokoka hawataki lakini Mbinguni wanataka kwenda; sijui nani kawaambia habari hiyo. Biblia inasema kutoka katika kitabu cha Warumi 6:23 kuwa "Kwa maana mshahara wa dhambi ni mauti bali karama ya Mungu ni uzima wa milele katika kristo Yesu Bwana wetu." Sasa iweje wewe uitumikie dhambi halafu ulipwe uzima wa milele badala ya mashahara wako ambao ni mauti. Hii ni sawa sawa kabisa na mfanyakazi wa T.R.A kwenda kudai mshahara wake UDA nina uhakika hawata mkubalia hata kidogo.

Hivyo wewe uliye mpokea Yesu kama Bwana na mwokozi wa maisha yako (umeokoka) mshike sana yesu kwa kuwa thawabu yako iko mbinguni Na wewe ambaye bado haujampokea yesu kristo kama Bwana na mwokozi wa maisha yako, nafasi ndio hii, unapopata ujumbe huu wa Dhumuni la Mungu kukuumba wewe ili upate neema ya kuingia Mbinguni na kuishi na Mungu wako milele na milele badala ya kwenda Jehanamu ya moto kuungua milele na milele.

Ukiwa umefuatilia somo hili kwa makini na Roho wa Mungu anazumngumza na wewe juu ya kumpokea Yesu ili uepuke gadhabu ya Mungu juu ya wanadamu waovu naomba useme maneno haya kwa kumaanisha toka ndani ya moyo wako ili Mungu akusamehe dhambi zako zote na kautakaswa kabisa ili uwe safi mbele zake.

"Mungu wangu na Baba yangu leo naja mbele zako nikiomba msamaha kwa maovu yangu yote niliyo kutenda tangu utoto wangu hata sasa.
Baba yangu wa Mbinguni nalitenda maovu kwa kutokujua kwangu lakini leo nimeamua kugeuka na kukutumikia wewe uliyeniumba.
Bwana Yesu kristo ninakuomba uingie ndani ya moyo wangu na ufanyike Bwana na mwokozi wa maisha yangu; Bwnana wangu naomba unikumbuke utakapokuja katika ufalme wako
- AMINA -


Ikiwa umesema maneno haya kwa kumaanisha kutoka ndani ya moyo jua sasa ya kwamba wewe umeokoka. Nakushauri utafute kanisa lolote la kiroho (watu waliookoka) watakusaidia kukulia vema wokovu wako.

MUNGU AKUBARIKI


Mwalimu
Mussa Daniel.


All Content © 2003
Gospel Power Center
Muta + Uswege Designs